Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Mheshimiwa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zuber bin Ally, amerejea nchini akitokea Jamhuri ya Kiarabu ya Misri alikohudhuria kikao cha kimataifa cha Mamufti kilichofanyika kwa muda wa siku mbili.
Akizungumza baada ya kurejea, Mufti amesema kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali yanayohusu changamoto na fursa za dunia ya sasa, ikiwemo matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI).
"Hatuwezi kuiepuka, kwani dunia imefika hapo kwa sasa. Hata hivyo, tusiipe nafasi kubwa katika kutatua matatizo ya masuala ya dini na elimu, kwani mwanzilishi wake ni mwanadamu. Zipo taarifa tunazoweza kuzitafuta kupitia AI, lakini sio kutegemea kila kitu kutoka kwake," alisema Mufti.
Aidha, Mufti alieleza kuwa kikao hicho pia kilijadili hali ya Wapalestina na njia zinazoweza kufanikisha amani ya kudumu katika eneo hilo.
"Tumejadili namna bora ya kumaliza mzozo huo kwa njia ya amani. Na tunawaombea ndugu zetu wa Gaza ili Mwenyezi Mungu awape amani na kumaliza mgogoro huu wa muda mrefu," aliongeza Mufti.
Your Comment